Thursday, 7 November 2013
TIKETI ZA P-SQUARE ZAGOMBEWA KAMA CHAKULA DAR
Uzwaji wa tiketi za kushuhudia Tamasha la Kundi maarufu la muziki wa kizazi kipya barani Afrika, P-Square, umeanza kufanyika jijini Dar es Salaam huku zikiuzwa kwa awamu tatu na kwa bei tatu tofauti.
Wadhamini wakuu wa tamasha hilo, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom Tanzania, wamekuwa wa kwanza kuanza kuuza tiketi hizo kupitia huduma ya M-pesa huku tiketi moja ikiuzwa kwa Sh. 30,000, zoezi ambalo litadumu hadi Novemba 17, mwaka huu.
Akizungumza jana Mikocheni jijini Dar es Salaam, Ofisa Masoko wa Kituo cha EATV, Alex Galinoma, alisema baada ya Novemba 17, tiketi hizo zitapanda bei na kuuzwa Sh. 35,000, safari hii zikiuzwa kwenye maduka mbalimbali jijini Dar es Salaam ambayo yatatangazwa baadaye.
"Bei hii itaendelea mpaka mchana wa siku ya tamasha, hivyo ukienda eneo la tamasha (Leaders Club) kununua tiketi mlangoni itakuwa ni Sh. 50,000," alifafanua Galinoma.
Kwa mara ya mwisho kundi hilo lilitua jijini Dar es Salaam, kwenye tamasha lililoandaliwa na Kituo cha EATV na kupewa jina la kibao chao kilichokuwa kikitamba wakati huo "Do Me".
Katika tamasha hilo lililofanyika Agosti 31, 2008 katika Viwanja vya Leaders Club, kiingilio kilikuwa ni Sh. 20,000 kwa onyesho la dakika 45 huku wakiimba kwa kuongozwa na CD "Playback".
Kwa mujibu wa Galinoma, safari hii wanamuziki hao watakuja na bendi nzima huku wakiimba 'laivu' kwa kutumia vyombo jukwaani kwa muda wa saa mbili bila kupumzika.
Galinoma alisema tamasha hilo la P-Square litaanza rasmi kuanzia saa 1:00 jioni mpaka saa 7:00 usiku, ili kuwapa mashabiki muda wa kupumzika na kuendelea na mambo mengine.
Milango ya Leaders Club itakuwa wazi kuanzia saa 12:00 jioni na mashabiki wataweza kuanza kuingia. Mashabiki wanashauriwa kufika mapema Leaders Club kwa sababu kutakuwa na ukaguzi wa kutosha na ulinzi mkubwa kwenye tamasha hili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment